ASAL Humanitarian Network (AHN)

Wito watolewa kwa Serikali Kuu na za Kaunti kushirikiana na jamii katika kaunti 23 zilizoathirika na ukame ili kudhibiti athari kwa wanawake, watoto na mifugo.

Mtandao wa Wahisani Wahimiza Serikali Kutatua Hali ya Ukame Nchini

ASAL Humanitarian Network yatoa tahadhari dhidi ya mzozo unaoendelea wa ukame unaowaathiri watu milioni 2.5 na kutishia usalama wa chakula na ustawi wa jamii.

Samburu, Kenya – Serikali imetakiwa kuchukua hatua za haraka na kushirikisha jamii katika kukabiliana na hali ya ukame inayozidi kuwa mbaya katika kaunti 23 za maeneo kame na nusu kame (ASAL) nchini Kenya, ambapo takriban watu milioni 2.5 wameathirika.

Jane Wariwe kutoka Samburu Women Trust, shirika mwanachama wa ASAL Humanitarian Network (AHN), ametoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya dharura ikiwemo ununuzi wa mifugo kupitia Kenya Meat Commission, ugavi wa chakula, na upatikanaji wa rasilimali muhimu zinazochochea migogoro ya kijamii katika maeneo yanayokumbwa na ukame.

“Kwa sasa wengi wameathirika na itakuwa vigumu hali ikiendelea kuwa hivi. Kina mama wetu na watoto wameathirika zaidi kwani ukosefu wa chakula, vituo vya afya hatuwezi fika na hata lishe kwa mifugo ni shida,” alisema Bi. Wariwe.

Bi. Wariwe ameeleza kuwa wanawake wajawazito na watoto ni kati ya makundi yaliyo katika hatari zaidi kutokana na ukosefu wa huduma muhimu za afya na lishe. Pia amesisitiza kuwa kuna haja ya kuimarisha usalama wa kijamii kwani ukame unasababisha ongezeko la mapigano kuhusu maji na maeneo ya malisho.

“Serikali za kaunti ziwe mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanashirikisha jamii katika mpango mzima wa kuhakikisha kuwa ukame na baa la njaa hauleti vurugu baina yao,” aliongeza.

AHN inaendelea kushirikiana na mashirika ya wanachama katika maeneo yaliyoathirika kuhakikisha kuwa sauti za jamii zinasikika, na kwamba mipango ya misaada inazingatia mahitaji ya ndani na heshima kwa uongozi wa jamii.